Martin Maranja Masese@IAMartin_
Uwepo wa Majaji Wakuu wawili wastaafu katika tume hiyo, ungetakiwa kuleta utimamu wa kisheria na kuziba mianya na mapengo ya kisheria. Ni bahati mbaya sana, hata raia wa kawaida wameyaona mapengo mengi.
Tume za uchunguzi wakati mwingine hufanya kazi kwa mujibu wa hadidu za rejea (terms of reference). Hata hivyo, ikiwa matokeo ya tume hiyo yanaathiri haki, mali, au sifa ya mtu, lazima kanuni za haki ya asili zitumike.
Ni jambo la kushangaza kuona mchakato wa kisheria au wa kijaji ukikwepa misingi ya kisheria na haki ya asili (natural justice), hususani unapoongozwa na watu wenye uzoefu mkubwa na ubonezi wa juu katika sheria.
Katika ulingo wa sheria ya ushahidi, haki ya kuhoji mashahidi (Cross-Examination) ni nyenzo muhimu zaidi ya kupata ukweli. Bila dodoso, mahakama (au hiyo tume) itakuwa inategemea simulizi za upande mmoja.
Katika sheria, cross-examination inajulikana kama injini kuu ya kisheria iliyowahi kuvumbuliwa kwa ajili ya kubaini ukweli (the greatest legal engine ever invented for the discovery of truth). Hutakiwi kuikwepa.
Bila mtuhumiwa au upande mwingine kupata fursa ya kumhoji shahidi, ushahidi huo unabaki kuwa wa upande mmoja (ex-parte). Tume inakuwa imejenga ukuta badala ya daraja katika kutafuta ukweli na haki.
Ushahidi wa aina hiyo kitaalamu unakosa kile kinachoitwa "Admissibility weight" kwa sababu haujafanyiwa jaribio la moto (fire-testing). Mchakato huo unakiuka misingi ya Haki ya Asili (Natural Justice).
Katika mahakama nyingi, ushahidi ambao haujapita kwenye dodoso huchukuliwa kama ushahidi dhaifu au wakati mwingine hukataliwa kabisa kwa sababu haujafanyiwa majaribio ya ukweli. Haujapimwa.
Dodoso husaidia kufichua uongo, upendeleo, au makosa ya kumbukumbu ya shahidi. Dodoso ndiyo njia ya kupima kama shahidi ni mwaminifu. Je, ana chuki? Je, ana maslahi ya kifedha? Maelezo yake yanalingana?
Bila maswali ya dodoso, uaminifu (credibility) wa shahidi hauwezi kuthibitishwa, na hivyo ushahidi wake hauwezi kuwa na probative value ya kumfunga mtu au kumwajibisha. Majaji wastaafu wanafahamu hilo.
Kupuuza dodoso ni kuubadili mchakato kutoka wa “kisheria” na kuwa wa “kiutawala” au “kisiasa,” jambo ambalo linafifisha dhana ya utawala wa sheria. Ndiyo wamekwepa kuwataja wahusika wa hayo mauaji.
Haki ya Kusikilizwa (Audi Alteram Partem). Hii ni nguzo ya kwanza ya haki ya asili—kwamba hakuna mtu anayepaswa kuhukumiwa bila kusikilizwa. Wametuhumiwa watu na makundi, hawahojiwa.
Right to Hearing: Ikiwa tume ilikusanya tuhuma dhidi ya watu fulani bila kuwapa nafasi ya kujitetea (right to be heard), ripoti au mapendekezo ya tume hiyo yanaweza kupingwa kisheria (procedural impropriety).
Kwa tume inayohusisha majaji wakuu wastaafu, matarajio ya umma na kisheria ni kwamba taratibu hizi zingefuatwa kwa ukamilifu ili kulinda heshima ya mchakato mzima. Badala yake, hatua zimerukwa
Unapokuwa na jopo lenye watu wenye weledi wa hali ya juu (kama Majaji Wakuu wastaafu), tegemeo ni kwamba wataulinda huu mwongozo wa haki ya asili (Natural Justice). Lakini katika tume hii, imekuwa tofauti.
Hao mnaosema walipanga, waliratibu, walifadhili waaandamanaji, mmewafikia na kuwahoji? Huo ushahidi usiokuwa na shaka ni ushahidi wa upande mmoja. Kwanini hamjawafikia waliotajwa, na kuwahoji?
Kitaalamu, Jaji anafahamu, hukumu au hitimisho lolote linalofikiwa bila kushirikisha upande unaotuhumiwa ni batili kisheria (null and void) endapo itatumika kama msingi wa kutoa adhabu/maamuzi ya kisheria.
MMM, Martin Maranja Masese, Mtikila.